Genesis 11

Mnara Wa Babeli

1Wakati huo dunia yote ilikuwa na lugha moja na msemo mmoja. 2 aWatu walipoelekea upande wa mashariki, wakafika kwenye tambarare katika nchi ya Shinari
Shinari ndio Babeli.
nao wakaishi huko.

3 cWakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tufyatue matofali na tuyachome vizuri kwa moto.” Walitumia matofali badala ya mawe, na lami kwa ajili ya kushikamanishia hayo matofali. 4 dNdipo wakasema, “Njooni, tujijengee mji wenye mnara ambao utafika hadi mbinguni, ili tujipatie jina tusije tukatawanyika usoni pa dunia yote.”

5 eLakini Bwana akashuka ili auone mji na mnara ambao wanadamu waliokuwa wanaujenga. 6Bwana akasema, “Ikiwa kama taifa moja wanaozungumza lugha moja wameanza kufanya hili, basi hakuna lolote watakalopanga kufanya ambalo halitawezekana kwao. 7 fNjooni, tushuke tuvuruge lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.”

8 gHivyo Bwana akawatawanya kutoka mahali pale kwenda katika dunia yote, nao wakaacha kuujenga huo mji. 9 hNdiyo maana pakaitwa Babeli, kwa sababu hapo ndipo Bwana alipoivuruga lugha ya dunia nzima. Kutoka hapo Bwana akawatawanya katika uso wa dunia yote.

Shemu Hadi Abramu

(1 Nyakati 1:24-27)

10 iHivi ndivyo vizazi vya Shemu.

Miaka miwili baada ya gharika, Shemu alipokuwa na miaka 100, akamzaa Arfaksadi.
11Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

12 jWakati Arfaksadi alipokuwa na miaka thelathini na mitano, akamzaa Shela. 13Baada ya Arfaksadi kumzaa Shela, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

14Shela alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Eberi. 15Shela baada ya kumzaa Eberi, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

16Eberi alipokuwa na miaka thelathini na minne, akamzaa Pelegi. 17Baada ya Eberi kumzaa Pelegi, aliishi miaka 430, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

18Pelegi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Reu. 19Baada ya Pelegi kumzaa Reu, aliishi miaka 209, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

20 kReu alipokuwa na miaka thelathini na miwili, akamzaa Serugi. 21Baada ya Reu kumzaa Serugi, aliishi miaka 207, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

22 lSerugi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Nahori. 23Baada ya Serugi kumzaa Nahori, aliishi miaka 200, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

24 mNahori alipokuwa na miaka ishirini na tisa, akamzaa Tera. 25Baada ya Nahori kumzaa Tera, aliishi miaka 119, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.

26 nTera alipokuwa na miaka sabini, akamzaa Abramu, Nahori na Harani.

Wazao Wa Tera

27 oHawa ndio wazao wa Tera.

Tera aliwazaa Abramu, Nahori na Harani. Harani akamzaa Lutu.
28 pTera alipokuwa bado hai, Harani akafa huko Uru ya Wakaldayo, nchi alimozaliwa. 29 qAbramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai, na mke wa Nahori aliitwa Milka; Milka na Iska walikuwa watoto wa Harani. 30 rSarai alikuwa tasa, hakuwa na watoto.

31 sTera akamchukua Abramu mwanawe, Lutu mwana wa Harani mwanawe, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka kwa pamoja katika Uru ya Wakaldayo kwenda nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakaishi huko.

32 tTera alikufa huko Harani akiwa na miaka 205.
Copyright information for SwhKC